Jumanne 2 Juni 2026 - 16:30
Maadamu Uvamizi Unaendelea, Muqawama Nao Utaendelea Kuwepo

Hawza/ Sheikh Ali Al-Khatib amewataka viongozi kutoweka matumaini yao kwa Marekani, ambayo inalenga kupitia mazungumzo ya moja kwa moja kuanzisha fitna ya ndani kwa ajili ya kumuokoa adui wa Kizayuni, na pia waachane na uamuzi wa kuwanyang’anya silaha Muqawama chini ya kauli ya “ukiritimba wa silaha.”

Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Sheikh Ali Al-Khatib, Naibu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Kiislamu la Mashia wa Lebanon, amewataka viongozi kutoweka matumaini yao kwa Marekani, ambayo inalenga kupitia mazungumzo ya moja kwa moja kuanzisha fitna ya ndani kwa ajili ya kumuokoa adui wa Kizayuni, na waachane na uamuzi wa kuwanyang’anya silaha Muqawama chini ya jina la “ukiritimba wa silaha.”

Alisisitiza kuwa: “Maadamu uvamizi unaendelea, Muqawama nao utaendelea kuwepo, na Lebanon haitakuwa tofauti na msingi huu wa kimantiki. Kwa hiyo, wale wanaounga mkono nadharia ya kunyang’anya silaha, maadamu uvamizi upo, waachane na matarajio yao.”

Sheikh Al-Khatib alisema: “Tunachokishuhudia leo ni vita kati ya nguvu zinazowakilisha kilele cha ufisadi; nguvu ambazo leo zinapaza sauti ya kuleta amani kwa kutumia nguvu, jambo ambalo maana yake ni kuwaangamiza wakazi wa Palestina, Lebanon, eneo la Kiarabu na Kiislamu, kuwatawala na kuwalazimisha kukubali utegemezi wa kisiasa, kiuchumi na kitamaduni, hii ni vita ya ustaarabu ambayo vikosi vya Muqawama, hususan Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, vinaiongoza peke yake; Iran imevunja nguvu na ushawishi wa Marekani, ambayo ni nguvu kubwa zaidi ya uovu duniani, pamoja na mtoto wake mwasi katika eneo hili.”

Aliendelea kusema: “Eneo hili liko katikati ya vita vinavyoitwa vita vya ‘uwepo’, na adui, licha ya msaada wa zana zake za ndani pamoja na himaya yake ya vyombo vya habari — himaya ya uongo, udanganyifu na upotoshaji — ambayo sasa ipo katika hali ya kufa na iko karibu na kuangamia, bado anajaribu kuonesha taswira ya nguvu na utawala wake kupitia uharibifu na mauaji anayoyafanya, kana kwamba bado ana ushawishi katika uwanja huu na ndiyo mshindi wa pambano hili.”

Naibu Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Mashia alieleza kwamba; vita halisi ni dhidi ya Marekani, na bila shaka yoyote imethibitika kushindwa kwake katika kuilazimisha Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kupiga magoti na kujisalimisha.

Alisema: “Iran leo ndiyo inayoainisha mwisho wa vita hivi katika nyanja zote kwa masharti yake yenyewe, na hakuna mtu yeyote anayeweza kuilazimisha Jamhuri ya Kiislamu kuachana na sharti lake la kusimamisha vita katika uwanja wa Lebanon, jambo ambalo litafikiwa kwa kuondoka kwa Marekani katika eneo hili.”

Sheikh Al-Khatib aliongeza: “Pia adui wa Kizayuni hatajijengea njia ya kujiokoa kwa kupanua ushawishi wake katika baadhi ya maeneo, bali atatoa nafasi zaidi kwa Muqawama kuwawinda wanajeshi wake na kuharakisha kusambaratika kwa jeshi lake, jambo ambalo Mkuu wa Majeshi yake mwenyewe amelikiri. Kwa hiyo wananchi wetu hawapaswi kuathiriwa na vita vya vyombo vya habari vinavyoendeshwa na adui kupitia mawakala na vibaraka wake.”

Aliongeza: “Viongozi wa Lebanon hawapaswi kuweka matumaini yao kwa Marekani ambayo inalenga kuanzisha fitna ya ndani kupitia mazungumzo ya moja kwa moja kwa ajili ya kumuokoa adui wa Kizayuni.”

Sheikh Al-Khatib aliwataka viongozi kutambua ukweli huu na waachane na maamuzi yao ya awali, hasa uamuzi wa kunyang’anya silaha za Muqawama, kwa sababu kanuni ya kawaida katika hali kama hii ni kwamba; uvamizi ndio unaozalisha Muqawama, si kinyume chake kama baadhi wanavyojaribu kueneza.

Katika hali hiyo, alisema, mjumbe wa Lebanon anaweza kutegemea Muqawama kama karata ya ushindi katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na adui.

Sheikh Al-Khatib alisisitiza kwamba: Mradi wa Israel wa kuiunganisha kusini mwa Lebanon na utawala huo vamizi unahitaji umoja na msimamo wa kitaifa miongoni mwa sehemu zote za Lebanon, kwa sababu: “Hatuamini na wala hatutaki kufikiria kwamba sehemu yoyote ya Lebanon inaweza kuridhia hata kipande kidogo cha ardhi ya Lebanon kitenganishwe kwa manufaa ya adui wa Kizayuni au wanaotamani ardhi ya Lebanon.”

Kwa hiyo aliwataka Walebanoni wote kuzingatia ukweli huu katika shughuli, hatua au harakati zozote za baadaye bila kujali aina, ukubwa au asili yake.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha